Mkataba wa Ivo waigawa Simba.

Ivo Mapunda.

Wakati  mkataba wa kipa chaguo la kwanza wa Simba, Ivo Mapunda, ukiwa unaelekea ukingoni mwisho wa msimu huu, viongozi wa klabu hiyo bado wanatofautiana kuhusu maamuzi ya kumpa mkataba mpya nyota huyo.
 
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinasema kwamba taarifa za kumpa Mapunda mkataba mpya si rasmi na hakuna kikao chochote kilichofanya maamuzi kuhusiana na kipa huyo ambaye aliwahi pia kuzidakia Yanga, Moro United, Prisons, St. George ya Ethiopia na Gor Mahia ya Kenya.
 
Chanzo hicho kiliendelea kusema kwamba viongozi wanaendelea kufanya mchakato wa kusaka kipa ambaye ataitumikia vyema timu hiyo katika msimu ujao na mwenye nafasi ni atakayekuwa na uzoefu wa mechi za kimataifa.
 
"Hakuna taarifa rasmi za Ivo kupewa mkataba mpya, tunazisikiasikia tu na hayo maneno yalianza baada ya mechi yetu dhidi ya Yanga," alisema kiongozi mmoja wa juu wa Simba.
 
Aliongeza kuwa klabu inahitaji kufanya maboresho katika nafasi mbili kwa ajili ya msimu ujao na kuitaja mojawapo ni ya kipa.
 
"Bado Simba hatujawa sawasawa langoni, huenda akaja mtu tofauti ambaye hajatarajiwa na atashirikiana na Manyika Junior na Casillas (Hussein Shariff)," kiongozi huyo aliongeza.
 
Alisema kwamba katika kujenga kikosi, ni lazima wachezaji wote waandaliwe kuanzia langoni mpaka safu ya ushambuliaji na hiyo ndio sababu ambayo inamuondoa Ivo kwenye mipango ya muda mrefu.
 
Gazeti hili lilipowasiliana na Katibu Mkuu wa Simba, Steven Ally, alisema hamna maamuzi yoyote ya kumsajili au kumuacha kipa huyo mkongwe.
 
Ally aliweka wazi kwamba bado uongozi haujaamua ni wachezaji gani wataachwa huku akiwataja Mapunda na beki Nassor Masoud 'Chollo' kuwa ndio ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu wa ligi.
 
"Kuna mazungumzo kidogo tumeshayaanza lakini hakuna maamuzi yaliyofikiwa hadi sasa, muda ukifika tutaweka wazi," alisema katibu huyo.
 
Simba ambayo msimu huu imetegemea nyota wake chipukizi waliopandishwa kutoka Simba B, iko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Bara na ikiamini inaweza kufanya 'maajabu' na kumaliza katika nafasi mbili za juu.
 
Wekundu hao wa Msimbazi wamekosa mara mbili nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Sambaza kwenye Google Plus

About HB Mtetezi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment